Jumapili. 08 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 15 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 19, 2024)  

Somo la 1

Isa 38:1–6, 21–22, 7–8

Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Kisha neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, name nitaulinda mji huu. Basi Isaya akasema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona. Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana? Jambo hili liwe ishara kwako itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

Wimbo wa Katikati

Isa 38:10–12, 16

Nalisema, katika usitawi wa siku zangu
Nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;
Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, Ee Bwana.

Nalisema, Sitamwona Bwana, yeye Bwana,
Katika nchi ya walio hai;
Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao
Wakaao duniani.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, Ee Bwana.

Kao langu limeondolewa kabisa,
Limechukuliwa kama hema ya mchungaji;
Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;
Atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;
Tangu mchana hata usiku wanimaliza.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, Ee Bwana.

Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi;
Na uhai war oho yangu u katika hayo yote;
Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, Ee Bwana.

Shangilio

Yn 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, name nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

Injili

Mt 12:1–8

Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

Maoni


Ingia utoe maoni