Masomo ya Misa
Jumamosi ya 15 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 20, 2024)
Mik 2:1–5
Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi Bwana asema hivi, Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, Sisi tumenyang’anyiwa kabisa; Yeye analibadili fungu la watu wangu; Jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu. Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa Kamba kwa kura katika mkutano wa Bwana.
Zab 10:1–4, 7–8, 14
Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali?
Kwa nini kujificha nyakati za shida?
Kwa kiburi chake asiye haki
Mnyonge anafuatiwa kwa ukali;
Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.
(K) Usiwasahau wanyonge, Ee Bwana.
Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake,
Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake
Asema, Hatapatiliza.
Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu.
(K) Usiwasahau wanyonge, Ee Bwana.
Kinywa chake kimejaa laana,
Na hila na dhuluma.
Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
Hukaa katika maoteo ya vijivi.
Mahali pa siri humwua asiye na hatia,
Macho yake humvizia mtu duni.
(K) Usiwasahau wanyonge, Ee Bwana.
Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri,
Uyatwae mkononi mwako.
Mtu duni hukuachia nafsi yake,
Maana umekuwa msaidizi wa yatima.
(K) Usiwasahau wanyonge, Ee Bwana.
Yn 14:23
Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.
Mt 12:14–21
Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Maoni
Ingia utoe maoni