Masomo ya Misa
Ijumaa baada ya Epifania (Ijumaa, Januari 10, 2020)
1Yoh 5:5-6, 8-13
Wapenzi: Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji wa damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Kwamaana wako watatu washuhudiao (mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani), Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.
Zab 147:12-15, 19-20
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi;
Neno lake lapiga mbio sana.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
1Tim 3:16
Aleluya, aleluya,
Sifa kwako, Ee Kristo, uliyehubiriwa katika mataifa; Sifa kwako, Ee Kristo, aliyeaminiwa katika ulimwengu.
Aleluya.
Lk 5:12-16
Ikawa Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao. Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.
Maoni
Ingia utoe maoni