Masomo ya Misa
Jumamosi baada ya Epifania (Jumamosi, Januari 11, 2020)
1Yn 5:14-21
Wapenzi: Huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.
Zab 149:1-6, 9
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.
Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa;
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Lk 7:16
Aleluya, aleluya
Nabii mkuu ametokea kwetu; Na Mungu amewaangalia watu wote
Aleluya
Yn 3:22-30
Siku ile, Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa. Maana Yohana alikuwa hajatiwa gerezani. Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso. Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.
Maoni
Ingia utoe maoni