Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. ALOIS GONZAGA (MTAWA) (Jumatano, Juni 21, 2017)
2 Kor. 9:6 – 11
Nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, haki yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu.
Zab. 112:1 – 2, 4 – 9
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Yak. 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
Mt. 6:1-6, 16 – 18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Basli wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena mfungapo, msiwe kama wanfiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao; ili waonekane na watu kuwa nafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Maoni
Ingia utoe maoni