Masomo ya Misa
Alhamisi ya 11 ya Mwaka (Alhamisi, Juni 22, 2017)
2 Kor. 11:1 - 11
Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami. Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye! Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nancho mitume walio wakuu. Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu. Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira? Naliwanyang’anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi. Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote nalijilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena nitajilinda. Kama vile vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya. Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.
Zab. 111: 1-4, 7-8
Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
(K) Matendo yako Bwana ni kweli na hukumu.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
(K) Matendo yako Bwana ni kweli na hukumu.
Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini,
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili.
(K) Matendo yako Bwana ni kweli na hukumu.
1The. 2:13
Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.
Mt. 6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliyembinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Maoni
Ingia utoe maoni