Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 5 ya Mwaka (Alhamisi, Februari 09, 2017)  

Somo la 1

Mwa 2:18-25

Bwana Mungu akasema tena, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.

Wimbo wa Katikati

Zab 128:1-5

Heri kila mtu amchaye Bwana, Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana

Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni Wakiizunguka meza yako.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana

Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni; Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako;
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana

Shangilio

Zab. 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.

Injili

Mk 7:24-30

Yesu alienda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba, akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika. Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake, akaja akamwangukia miguuni pake. Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katika binti yake. Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto, na kuwatupia mbwa. Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya watoto. Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako. Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.

Maoni


Ingia utoe maoni