Jumapili. 19 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Scholastika, Bikira (Ijumaa, Februari 10, 2017)  

Somo la 1

Mwa 3:1-8

Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.

Wimbo wa Katikati

Zab 32:1-2, 5-7

Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu,
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K)Heri aliyesamehewa dhambi

Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
(K)Heri aliyesamehewa dhambi

Kwa hiyo kila mtu mtauwa Akuombe wakati unapopatikana.
Hakika maji makuu yafurikapo, Hayatamfikia yeye.
(K)Heri aliyesamehewa dhambi

Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
Utanizungusha nyimbo za wokovu.
(K)Heri aliyesamehewa dhambi

Shangilio

Zab. 119:34

Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

Injili

Mk 7:31-37

Yesu akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

Maoni


Ingia utoe maoni