Jumapili. 19 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 5 ya Mwaka (Jumatano, Februari 08, 2017)  

Somo la 1

Mwa. 2:4 – 9, 15 – 17

Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyesha nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.

Wimbo wa Katikati

Zab. 104:1 – 2, 27 – 30

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na adhama.
Umejivika nuru kama vazi;
Umezitandika mbingu kama pazia;
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Hao wote wanakungoja Wewe,
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
Wewe huwapa,
Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema;
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wan chi.
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Shangilio

Zab. 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.

Injili

Mk. 7:14 – 23

Yesu aliwaita makutano tena, akawaambia, NIsikieni nyote na kufahamu. Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.

Maoni


Ingia utoe maoni