Jumapili. 05 Mei. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA WATAKATIFU BASILI MKUU NA GREGORI WA (Jumatatu, Januari 02, 2017)  

Somo la 1

1Yn 2:22-28

Wapenzi: ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia. Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele. Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake. Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake katika kuja kwake.

Wimbo wa Katikati

Zab. 98:1-4

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.

Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.

Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Siku takatifu imetung’aria: Enyi mataifa njoni mkambwabudu Bwana: Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.

Injili

Yn. 1:19-28

Na huu ndio ushuhuda wake Yohane, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristu. Wakamwuliza, Ni nani basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohane akawajibu akisema, Mimi nabatiza na maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohane akibatiza.

Maoni


Ingia utoe maoni