Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jina Takatifu la Yesu (Jumanne, Januari 03, 2017)  

Somo la 1

1 Yoh 2:29-3:6

Wapenzi; kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye. Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu. Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.

Wimbo wa Katikati

Zab 98:1, 3-6

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu

Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote, Inueni sauti,
imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu

Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu.
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu

Injili

Yn 1:29-34

Siku ile , Yohane alimwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohane akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni