Masomo ya Misa
Sikukuu ya Mt. Toma, Mtume (Jumatano, Julai 03, 2024)
Efe 2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
Zab 117
Aleluya.
Enyi mataifa wote, mhimidini.
enyi watu wote, mhimidini.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili.
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele.
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili.
Yn 20:29
Aleluya, aleluya,
Wewe, Tomaso, kwa kuwa umeniona, umesadiki, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.
Yn 20:24-29
Mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Maoni
Ingia utoe maoni