Masomo ya Misa
Alhamisi ya 13 ya Mwaka (Alhamisi, Julai 04, 2024)
Amo 7:10–17
Amazia kuhani wa Betheli, alipeleka habari kwa Yeroboamu, mfalme wa Israeli, akisema, Amosi amefanya fitina juu yako kati ya nyumba ya Israeli; nchi haiwezi kustahimili maneno yake yote. Kwa maana Amosi asema hivi, Yeroboamu atakufa kwa upanga, na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali, hali ya kufungwa, atoke katika nchi yake. Tena Amazia akamwambia Amosi, Ewe mwona, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme, nayo ni nyumba ya kifalme. Ndipo Amosi akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye Bwana akanitwaa, katika kufuatana na kundi; Bwana akaniambia, Enenda uwabarie watu wangu Israeli. Basi, sasa lisikie neno la Bwana; Wewe unasema, Usitabiri, Usitabiri juu ya Israeli, wala usitoe neno lako juu ya nyumba ya Isaka; kwa hiyo, Bwana asema hivi, Mke wako atakuwa kahaba mjini, na wana wako na binti zako wataanguka kwa upanga, na shamba lako litagawanywa kwa kamba; na wewe mwenyewe utakufa katika nchi iliyo najisi; na bila shaka Israeli atachukuliwa mbali hali ya kufungwa kutoka nchi yake.
Zab 19:7–10
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
humtia mjinga hekima.
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
(K) Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
kinadumu milele.
(K) Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
Hukumu za Bwana ni kweli,
zina haki kabisa.
(K) Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali.
(K) Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
Zab 119:105
Aleluya, aleluya.
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
Mt 9:1-8
Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu; umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (akamwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
Maoni
Ingia utoe maoni