Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Malaika Walinzi (Jumatatu, Oktoba 02, 2023)  

Somo la 1

Zek 8:1-8

Neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu. Bwana asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa Bwana wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu. Bwana wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake. Bwana wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema Bwana wa majeshi. Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi; nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.

Wimbo wa Katikati

Zab 102:15-20, 28, 21-22

Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Wana wa watumishi wako watakaa,
Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.
Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
Na sifa zake katika Yerusalemu,
Pindi mataifa watapokusanyika pamoja,
Falme nazo ili kumtumikia Bwana.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Injili

Mt 18:1-5, 10

Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni