Jumatatu, Oktoba 02, 2023
Jumatatu, Oktoba 2, 2023.
Juma la 26 la Mwaka
Kumbukumbu ya Malaika Walinzi
Kut 23: 20-23;
Zab 90: 1-6, 10-11;
Mt 18: 1-5, 10
MALAIKA –ULINZI WA MUNGU KWETU
Kanisa Katoliki linafundisha tunapaswa kukumbuka ni kwa jinsi ghani ilikuwa lengo la Mungu la kuwaweka malaika walinzi kwa ajili ya kuwalinda wanadamu na kuwaongoza, kwa kila mwanadamu, ili wasije wakaanguka katika hatari kubwa. Masomo yanatoa mwanga wa ujumbe huu.
Katika somo la kwanza tunasikia kwamba Waisraeli walipewa malaika wa kuwaongoza katika safari yao, na kwamba kama watamtii Mungu atawapa ushindi juu ya maadui zake. Katika somo la Injili tunajifunza kwamba watoto hawapaswi kudharauliwa au kukataliwa, wana thamani mbele ya Mungu kwani malaika wao wapo mbele za Mungu daima. Katika maisha yetu ya kila siku malaika wa Mungu huongea nasi kutuelekeza kuacha njia mbaya na kugeukia mema, au kwa kutuweka katika hali ambazo tutajifunza kuacha ubaya kwa tukio fulani au kwa njia ya dhamiri zetu lakini pia aweza kutumia watu watuambie tuache jambo fulani kuepuka ubaya, lakini daima hawaingilii uhuru kamili wa mtu. Lakini tunabarikiwa sana tunapo amua kusikiliza sauti yao ya kutuambia tuache ubaya na kujeukia mema.
Tafakari, leo, juu ya zawadi ya malaika wako mlinzi. Huyu kiumbe wa Mungu aliumbwa ili akuhudumie wewe na baadaye akufikishe Mbinguni. Ongea na malaika wako leo. Kwa kutegemea maombi ya malaika wako ruhusu huyu Malaika Mtakatifu wa Mungu azungumze na wewe kwa njia ya neema kuu.
Sala:
Malaika wa Mungu mpendwa, ambaye kwa njia ya mapendo yake mimi nipo hapa, endelea kuwa nami daima, kuniangazia na kunikinga amina. Malaika wa Mungu , mniombee. Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni