Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 26 ya Mwaka (Jumapili, Oktoba 01, 2023)  

Somo la 1

Eze 18:25-28

Bwana ameniambia hivi: Ninyi mwasema, Njia ya Bwana si sawa. Sikiliza sasa, Enyi nyumba ya Israeli; Je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakati, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika, ataishi, hatakufa.

Wimbo wa Katikati

Zab 25:4-9

Ee Bwana, unijulishe njia zako, 
Unifundishe mapito yako;
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha:
Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.
(K) Kumbuka rehema zako, Ee Bwana.

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala mausi yangu,
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. 
(K) Kumbuka rehema zako, Ee Bwana.

Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha njia wenye dhambi.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu.
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Kumbuka rehema zako, Ee Bwana.

Somo la 2

Flp 2:1-11

Ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako matulizo yoyote ya mapenzi, ukiwako ushirika wowote wa Roho, ikiwako huruma yoyote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. Msitende neno lolote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo yaw engine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Shangilio

Yn 15:15

Aleluya, aleluya,
Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.

Injili

Mt 21:28-32

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee, Mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Bwana Yesu akawaambia, Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini; nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

Maoni


Ingia utoe maoni