Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 14 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 14, 2023)  

Somo la 1

Mwa 46 :1-7, 28-30

Israeli alisafiri pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha lena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao, na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri. Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake, kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.

Wimbo wa Katikati

Zab 37 :3-4, 18-19, 27-28, 39-40

Umtumaini Bwana ukatende mema,
ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Bwana anazijua siku za wakamilifu,
na urithi wao utakuwa wa milele.
Hawataaibika wakati wa ubaya,
na siku za njaa watashiba.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Jiepue na uovu, utende mema,
na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
wala hawaachi watauwa wake.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Na wokovu wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Shangilio

Yak 1:21

Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.

Injili

Mt 10:16-23

Yesu aliwaambia mitume wake: Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

Maoni


Ingia utoe maoni