Masomo ya Misa
Alhamisi ya 14 ya Mwaka (Alhamisi, Julai 13, 2023)
Mwa 44: 18-21, 23-29; 45 :1-5
Yuda alimkaribia Yusufu akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. Wewe, bwana wangu ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! mnaye baba, au ndugu? Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena. Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka; maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. Mtumwa wako, Baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alimzalia wana wawili; mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema. mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha za watu.
Zab 105:16-21
Bwana aliita njaa iijilie nchi,
akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu aliuzwa utumwani.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.
Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.
Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa Bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote.
(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.
Ebr 4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
Mt 10:7-15
Yesu aliwaambia mitume wake: Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni imekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; mana Mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote u kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawambia, Itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.
Maoni
Ingia utoe maoni