Masomo ya Misa
Jumamosi ya 14 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 15, 2023)
Mwa 49:29-33; 50:15-25
Yakobo aliwaamuru wanawe: Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia. Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea; shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa bani Hethi. Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; nave atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Nakuomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha, na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi lusuru miaka mia na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha kutoka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akisema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.
Zab 105:1-4, 6-7
Aleluya.
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake,
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Jisifuni kwa jina lake lakatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake siku zote.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake,
enyi wana wa Yakobo wateule wake.
Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu,
duniani mwote mna hukumu zake.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
1Pet 1 :25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
Mt 10:24-33
Yesu aliwafundisha mitume wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli; je! si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni