Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. BONIFASI (ASKOFU NA SHAHIDI) (Jumatatu, Juni 05, 2023)
Tob. 1:1, 2:1-8
Kitabu cha habari za Tobiti, bin Tobieli, bin Ananieli, bin Adueli, bin Gabaeli, wa uzao wa Asieli, wa kabila ya Naftali. Zamani za Shalmanesa, mfalme wa Waashuru, huyu alichukuliwa mateka kutoka Tisbe, ulioko upande wa kuume wa Kadeshi-Naftali katika Galilaya, upande wa juu wa Asheri. Mimi Tobiti, nilipofika nyumbani kwangu, na kurudishiwa mke wangu Ana na mwanangu tobia, kwenye sikukuu ya Pentekoste, iliyo siku takatifu ya juma saba, naliandaliwa chakula kizuri, nikakaa kitako nile. Ndipo nilipoona nyama tele, nikamwambia mwanangu, Nenda ukamlete mtu maskini yeyote utakayemwona miongoni mwa ndugu zetu amkumbukaye Bwana. Haya! Nakungojea. Akarudi, akasema, Baba, kuna mtu mmoja wa taifa letu amenyongwa; akatupwa sokoni. Mara, kabla sijadiriki kuonja chakula chochote, naliondoka kwa haraka, nikaenda nikamchukua, nikampeleka katika chumba hata kuchwa kwa jua. Kisha nikarudi nikaoga, nikala chakula changu kwa msiba, huku nikiukumbuka ule unabii wa Amosi, kusema, Nitageuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio. Kwa hiyo nikalia; na jua lilipokwisha kuchwa, nalikwenda nikachimba kaburi, nikamzika. Lakini jirani zangu walinidhihaki, wakasema, Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia; na kumbe! Anazika maiti tena.
Zab. 112:1 – 6
Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha Wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu amchaye Bwana.
Au: Aleluya.
Nyumbani mwake mna utajiri na mali,
Na haki yake yakaa milele.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
(K) Heri mtu amchaye Bwana.
Au: Aleluya.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele.
(K) Heri mtu amchaye Bwana.
Au: Aleluya.
Zab. 119:105
Aleluya, aleluya.
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.
Mk. 12:1-12
Yesu alisema na Mafarisayo kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma, mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha -za kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.
Maoni
Ingia utoe maoni