Masomo ya Misa
Sherehe ya Utatu Mtakatifu (Jumapili, Juni 04, 2023)
Kut 34:4b-6, 8-9
Musa aliinuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake. Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.
Dan 3:52-56
Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu:
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele
Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kurukuzwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele
Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi;
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele
2Kor 13:11-14
Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. Salimianeni kwa busu takatifu. Watakatifu wote wawasalimu. Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.
Ufu 1:8
Aleluya, aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu ambaye yupo, aliyekuwako na atakayekuja.
Aleluya
Yn 3:16-18
Yesu alimwambia Nikodemu: Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni