Ijumaa. 26 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 19 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 12, 2022)  

Somo la 1

Eze 16:59–63

Bwana Mungu asema hivi; Nitakutenda vile vile kama ulivyotenda, uliyekidharau kiapo kwa kulivunja agano. Walakini nitalikumbuka agano langu nililolifanya pamoja nawe, katika siku za ujana wako, nami nitaweka imara agano la milele pamoja nawe. Hapo ndipo utakapozikumbuka njia zako, na kutahayarika, hapo utakapowakaribisha maumbu yako, walio wakubwa wako na wadogo wako; nami nitakupa hao wawe binti zako, lakini si kwa agano lako. Nami nitaweka imara agano langu nawe; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; upate kukumbuka, na kufadhaika, usifumbue kinywa chako tena, kwa sababu ya aiba yako; hapo nitakapokusamehe yote uliyoyatenda, asema Bwana Mungu.

Wimbo wa Katikati

Isa 12:2–6

Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu
Na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
(K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo.

Basi, kwa furaha mtateka maji
Katika visima vya wokovu.
Na katika siku hiyo mtasema,
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka.
(K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo.

Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
(K) Hasira yako imegeukia mbali, nawe unanifariji moyo.

Shangilio

Ebr 4:12

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.

Injili

Mt 19:3–12

Mafarisayo walimwendea Yesu wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha? Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. Nami nawambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. Wanafunzi wake wakamwambia, Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. Lakini yeye akawaambia, Si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa. Maana wako matowashi waliozaliwa hali hiyo toka matumobni mwa mama zao; tena wak omatowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi; tena wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.

Maoni


Ingia utoe maoni