Masomo ya Misa
Jumamosi ya 19 ya Mwaka (Jumamosi, Agosti 13, 2022)
Eze 18:1–10, 13, 30–32
Neno la Bwana likanijia tena, kusema, Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? Kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa. Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki; hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake; wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi; ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yoyote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati aya mtu na mwenzake; tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mungu. Walakini akizaa mwana aliye mnyang’anyi, mwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo, naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi badala ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake. Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana Mungu. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na rohoho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana Mungu; basi ghairini, mkaishi.
Zab 51:10–13, 16–17
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.
(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
1Pet 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hili ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
Mt 19:13–15
Yesu aliletewa watoto wadogo ili aweke mikono yake juu yao na kuwaombea; wanafunzi wake wakawakemea. Lakini Yesu akasema, Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao. Akaweka mikono yake juu yao, akatoka huko.
Maoni
Ingia utoe maoni