Masomo ya Misa
Jumatano ya 17 ya Mwaka (Jumatano, Julai 27, 2016)
Yer 15:10, 16-21
Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu? Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.
Zab 59:2-4, 10-11, 17-18
Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
Uniponye nao wafanyao maovu, Uniokoe na watu wa damu.
(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu
Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; Wenye nguvu wamenikusanyikia;
Ee Bwana, si kwa kosa langu, Wala si kwa hatia yangu.
(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu
Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu
Mungu wa fadhili zangu atanitangulia, Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu.
(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu
Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi, Nitaziimba fadhili zako kwa furaha.
Kwa kuwa ndiwe uliyekuwa ngome yangu, Na makimbilio siku ya shida yangu.
(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu
Ee nguvu zangu, nitakuimbia kwa furaha,
Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu, Mungu wa fadhili zangu.
(K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu
Yn 15:15b
Aleluya, Aleluya
Ninyi nimewaita rafiki; Asema Bwana, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu
Aleluya
Mt 13:44-46
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.
Maoni
Ingia utoe maoni