Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Watakatifu Joackim na Anna wazazi wa Bikira Maria (Jumanne, Julai 26, 2016)  

Somo la 1

Yer 14:17-22

Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka. Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa. Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu! Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi. Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako, kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi. Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, Ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.

Wimbo wa Katikati

Zab 79:8-9, 11, 13

Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, ee Bwana.

Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, ee Bwana.

Kuugua kwake aliyefungwa Na kuingie mbele zako.
Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi.
(K) Kwa ajili ya utukufu wa jina lako, utusaidie, ee Bwana.

Shangilio

.

Aleluya, aleluya
Neno la Mungu ni mbegu, na Kristu ndiye mpanzi, wote watakaokuja kwake wataishi milele.
Aleluya

Injili

Mt 13:36-43

Yesu aliwaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.

Maoni


Ingia utoe maoni