Masomo ya Misa
Dominika ya 17 ya Mwaka (Jumapili, Julai 24, 2016)
Mwa 18:20-32
Bwana alisema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.
Zab 138:1-3, 6-8
Nitakushukuru kwa moyo wangu wote, Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
(K)Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu
Nitalishukuru jina lako, Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako, Kuliko jina lako lote.
Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
(K)Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu
Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu,
Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.
Nijapokwenda kati ya shida utanihuisha,
Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
(K)Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Bwana atanitimilizia mambo yangu;
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako.
(K)Siku ile niliyokuita uliniitikia, Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu
Kol 2:12-14
Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu. Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;
Yn 14:23
Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atashika neno langu, na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya
Lk 11:1-13
Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]. Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake. Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?
Maoni
Ingia utoe maoni