Masomo ya Misa
Ijumaa ya 21 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 30, 2019)
1The 4:1-8
Ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.
Zab 97:1-2, 5-6, 10-12
Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Enyi wenye haki, mfurahini Bwana.
Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake.
(K) Enyi wenye haki, mfurahini Bwana.
Enyi mmpendao Bwana, uchukieni uovu;
Huwalinda nafsi zao watauwa wake,
Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.
(K) Enyi wenye haki, mfurahini Bwana.
Nuru imemzukia mwenye haki,
Na furaha wanyofu wa moyo.
Enyi wenye haki, mmfurahieni Bwana,
Na kulishukuru jina lake takatifu.
(K) Enyi wenye haki, mfurahini Bwana.
Mt 25:1-13
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.
Maoni
Ingia utoe maoni