Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kufa kwa Shahidi Mt. Yohane Mbatizaji (Alhamisi, Agosti 29, 2019)  

Somo la 1

Yer 1:17-19

Neno la Bwana lilimjia kusema, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.

Wimbo wa Katikati

Zab 71:1-6, 15, 17

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.


Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa;
maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Injili

Mk 6:17-29

Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Maoni


Ingia utoe maoni