Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 7 ya Pasaka (Alhamisi, Mei 12, 2016)  

Somo la 1

Mdo 22:30; 23:6-11

Wakati ule Jemadari alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.

Wimbo wa Katikati

Zab 16:1-2, 7-11

Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
(K)Mungu unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia wewe.

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K)Mungu unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia wewe.


Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
(K)Mungu unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia wewe.


Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
(K)Mungu unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia wewe.

Shangilio

Yn 17:21

Aleluya, Aleluya
Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako;
ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma asema Bwana
Aleluya

Injili

Yn 17:20-26

Siku ile Yesu alisali akisema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

Maoni


Ingia utoe maoni