Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 7 ya pasaka (Ijumaa, Mei 13, 2016)  

Somo la 1

Mdo 25: 13-21

Siku zile,Agripa mfalme na Bernike wakafika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumu nikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.

Wimbo wa Katikati

Zab 103:1-2, 11-12, 19-20


Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam,
vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K)Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.


Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
(K)Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.

Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake
(K)Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.

Shangilio

Yn 14:26


Aleluya, aleluya
Roho Mtakatifu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Aleluya

Injili

Yn 21:15-19

Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonyesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo akamwambia, Nifuate.

Maoni


Ingia utoe maoni