Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 26, 2020

Jumatatu, Oktoba 26, 2020,
Juma la 30 la Mwaka wa Kanisa

Ef 4:32 – 5:8;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 13:10-17

HURUMA YA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo miongoni mwa msisitizo ni Paulo kuwaambia wakristo wa Efeso kwamba waishi vyema na wawe na kauli njema toka kinywani mwao, maneno machafu yasisikie kamwe mdomoni mwao. Maneno yao yawe ya kutia moyo na yenye kuponya matatizo ya watu na si kuwakatisha tamaa.

Ndugu zangu, maneno mabaya naya kudharau yamewaumiza wengi; wengi wamepata magonjwa na kujeruhiwa vibaya kwa sababu ya maneno mabaya. Kinyume chake ni kwamba maneno mazuri yameweza kuwa uponyaji kwa wengi. Sisi ndugu zangu kama wakristo maneno na majibu yetu lazima yawe ya kutia moyo kwa yeyote. Huu ndio ukarimu tunaoweza kuwaonyesha watu hata kama ikitokea hatuna pesa za kuwapa watu. Kauli nzuri ndio ukarimu wetu na msaada wetu kwa watu. Kauli yangu nzuri inatosha.

Kingine pia ni kutumia vinywa vyetu vyema kwenye kuongea maneno mazuri. Wengi wetu hasa vijana tunatumia muda mwingi kuongea habari zisizofaa; kinywa chetu kinamtangaza shetani zaidi kuliko Mungu. Tubadilike. Tusiache shetani atamalaki zaidi ndani ya vinywa vyetu; akitawale kama chake.

Katika injili, tunakutana na mama akiponywa leo na baada ya kuponywa anamtukuza Mungu. Cha ajabu ni kwamba anapoponywa na kuanza kumtukuza tu Mungu, mkuu wa sinagogi anakasirika. Yeye anashindwa kuangalia lile jambo zuri kwamba Mungu ametukuzwa bali anaishia kukasirika na kusema sheria ya sabato imevunjwa.

Ndivyo tulivyo kwa wengi wetu. Mara nyingi tukitenda jambo, tunakasumba ya kuangalia hasi kuliko chanya. Huu ni ugonjwa wa wengi wetu. Jamani kuna na upande chanya na tuombe tuwe watu wa kuona upande chanya pia. Tumehukumu wengi kwa sababu ya kuangalia upande mmoja tu. Tufungue macho jamani. Kuna pande mbili pia na ziangalie zote pia. Wengi tumeshindwa kuishi na wenzetu, na kugombana nao kila siku kwa sababu ya kuangalia upande mmoja tu. Hatujui kwamba kuna pande mbili pia tunazopaswa kuziangalia. Ebu tufungue macho zaidi na kuangalia pande zote mbili kama maisha yetu hayatabadiliika na kuwa tofauti kabisa na uhusiano wetu na watu kubadilika.

Maoni


Ingia utoe maoni