Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 30 ya Mwaka (Jumatatu, Oktoba 26, 2020)  

Somo la 1

Efe 4:32–5:8

Iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wala kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu. Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi. Basi msishirikiane nao. Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru.

Wimbo wa Katikati

Zab 68:1, 3, 5–6, 19–20

Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki; wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa.

Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa.
(K) Mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa.

Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo,
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki.
Bali njia ya wasio haki itapotea.
(K) Mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa.

Shangilio

Yak 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.

Injili

Lk 13:10-17

Siku ya sabato Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akamjibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, Je! Hamfungi ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.

Maoni


Ingia utoe maoni