Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mt. Klara (Jumamosi, Agosti 11, 2018)
Hab 1:12-2:4
Ee Bwana, Mungu wangu, mtakatifu wangu, wewe si wa milele? Hatutakufa. Ee Bwana, umemwandikia hukumu, nawe, Ee Jabali, umemweka imara ili aadhibishwe. Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao kwa hila; na kunyamaza kimya, hapo mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye; na kufanya wanadamu kuwa kama samaki wa baharini, kama vitu vitaambavyo, ambavyo havina mtawala? Yeye huwatoa wote kwa doana yake, huwakamata katika wavu wake, na kuwakusanya katika juya lake; ndiyo sababu afurahi na kupendezwa. Kwa sababu hiyo huutolea wavu wake sadaka na kulifukizia uvumba juya lake; kwa sababu kwa vitu vile fungu lake limenona, na chakula chake kimekuwa tele. Je! Atawatoa walio katika wavu wake, asiache kuwaua watu wa mataifa daima? Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu. Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia. Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa Imani yake.
Zab. 9:7 – 12
Bwana atakaa milele,
Ameweka kiti chake tayari kwa hukumu.
Naye atauhukumu ulimwengu kwa haki;
Atawaamua watu kwa adili.
(K) Wewe Bwana, hukuwaacha wakutafutao.
Bwana atakuwa ngome kwake aliyeonewa,
Naam, ngome kwa nyakati ya shida.
Nao wakujuao jina lako wakutumaini Wewe,
Maana Wewe, Bwana, hukuwaacha wakutafutao.
(K) Wewe Bwana, hukuwaacha wakutafutao.
Mwimbieni Bwana akaaye Sayuni,
Yatangazeni kati ya watu matendo yake.
Maana mlipiza kisasi cha damu awakumbuka,
Hakukisahau kilio cha wanyonge.
(K) Wewe Bwana, hukuwaacha wakutafutao.
Yn. 10: 27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Mt. 17:14 – 20
Mtu mmoja alimjia Yesu, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nayi hata lini? Mleteni huku kwangu. Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa Imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na Imani kiasi cha punji ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowekana kwenu.
Maoni
Ingia utoe maoni