Jumatano. 27 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Agosti 11, 2018

Jumamosi, Agosti, 11, 2018,
Juma la 18 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mt. Klara,

Hab 1:12 – 2:4;
Zab 9: 8-13;
Mt 17: 14-20.

TUOMBEANE

Mtu mmoja alikuja kwa Yesu na kupiga magoti na kumuomba “Bwana mwanangu ni mgonjwa na anapagawa na pepo mchafu na mara nyingi humwangusha kwenye moto na maji ili amwangamize. Nimemleta kwa wafuasi wako wasiweze kumponya”. Yesu alimtoa pepo kutoka kwa kijana yule. Kilio hiki cha huyu mtu aliyeenda kwa Yesu chaweza kuwa kilio cha wazazi sasa wanaosali juu ya watoto wao walio anguka kwenye moto na maji ya dhambi na wanataka kuangamia. Na wazazi wengi wameishia kupiga magoti mbele ya Mungu. Katika sehemu hii ya Injili inamuonesha huyu Baba kama mtu jasiri asiye kata tamaa. Pengine angeweza kumtazama mtoto wake kama mtu ambaye hapaswi kutazamwa kwa karibu au kwamba sio muhimu. Lakini cha ajabu huyu Baba hakuja tu kwa Yesu bali alipiga magoti mbele ya Yesu na kumuomba Yesu amuonee huruma. Alikuwa na tumaini juu ya mtoto wake na kwamba kwa Yesu kuna kitu, na hivyo kwa tumaini lake akapata neema na uponyaji kwa ajili ya mtoto wake. Nasi tusikate tamaa kuwaombea watoto wetu.
Wafuasi kwa kuwaponya wengi katika safari yao ya kitume, wanashangaa kwanini walishindwa kumtoa pepo huyo. “kwasababu walikuwa na Imani haba”. Yesu aliwaambia. “Hata chembe kidogo kabisa ya Imani kwa Mungu inauwezo wakuhamisha milima”. Imani hiyo ikiwa imepambwa na upendo wa ndani, ndicho kinacholeta furaha na amani katika macho yetu na amani katika maisha yetu hata katika nyakati ngumu katika maisha yetu.

Leo sehemu hii inatufunulia ukweli kwamba tunapaswa kuombeana. Tunapaswa kuwaombea walio karibu na sisi na walio katika uhitaji wetu. Hakuna aliye juu ya tumaini. Yote yanawezekana kwa njia ya sala na Imani.

Tafakari kama kuna mtu katika maisha yako ambaye umeanza kukata tamaa naye. Pengine umejaribu sana na huyo mtu ndio kwanza yupo mbali na Mungu. Kwa njia hiyo uwe na hakika kwamba wito wako ni kwa ajili ya kumuombea huyo mtu. Pengine umeitwa kumuombea sio kwa haraka haraka lakini kwa utulivu na kuzama katika Imani. Tambua Yesu ni jibu naye ndiye mwenye uwezo wa kujibu kila kitu. Muweke huyo mtu kwenye huruma ya Mungu. Usikate tamaa, kuwa na tumaini kwamba Mungu anauwezo wakuleta tumaini na kubadili maisha.

Sala:
Bwana, nionee huruma mimi, familia yangu na wale wote wanahitaji. Naomba ulete uponyaji, utakatifu na fanya upya maisha ndani mwangu, katika familia yangu na marafiki walio karibu yangu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni