Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 3 ya Pasaka (Alhamisi, Aprili 19, 2018)  

Somo la 1

Mdo. 8:26-40

Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo. Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma? Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye. Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake. Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi. Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine? Filipo akafunua kinywa chake, naye, akakianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi. Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria.

Wimbo wa Katikati

Zab. 66:8-9, 16-17, 20

Enyi mataifa, mtukuzeni Mungu wetu,
Itangazeni sauti ya sifa zake;
Aliyeiweka nafsi yetu katika uhai,
Wala hakuuacha mguu wetu usogezwe.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Njoni sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Nalimwita kwa kinywa changu,
Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulinzi wangu.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu;
Wala kuniondolea fadhili zake.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Shangilio

Yn. 20: 29

Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.

Injili

Yn. 6:44-51

Yesu aliwaambia Wayahudi: Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

Maoni


Ingia utoe maoni