Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatato ya 3 ya Pasaka (Jumatano, Aprili 18, 2018)  

Somo la 1

Mdo 8:1-8

Siku ile kulitukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

Wimbo wa Katikati

Zab. 66:1-7

Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake,
Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele;
Macho yake yawaangalia mataifa;
Waasio wasijitukuze nafsi zao.
(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.

Shangilio

Yn. 10:27

Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.

Injili

Yn. 6:35-40

Yesu aliwaambia: Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmjoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

Maoni


Ingia utoe maoni