Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaaya 5 ya Mwaka (Ijumaa, Februari 09, 2018)  

Somo la 1

1 Fal 11:29-32; 12:19

Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi, (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli); Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo.

Wimbo wa Katikati

Zab 81:9-14

Usiwe na mungu mgeni ndani yako;
Wala usimsujudie mungu mwingine.
Mimi ndimi Bwana, Mungu wako,
Niliyekupandisha toka nchi ya Misri;
(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako Isikieni sauti yangu.

Lakini watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu,
Wala Israeli hawakunitaka.
Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao,
Waenende katika mashauri yao.
(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako Isikieni sauti yangu.

Laiti watu wangu wangenisikiliza,
Na Israeli angeenenda katika njia zangu;
Ningewadhili adui zao kwa upesi,
Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu;
(K) Mimi ndimi Bwana Mungu wako Isikieni sauti yangu.

Shangilio

Mdo. 16:14

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana ufungue moyo wetu, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.

Injili

Mk 7:31-37

Yesu alitoka katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli. Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono. Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka. Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri. Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari; wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

Maoni


Ingia utoe maoni