Jumatatu. 20 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 27 ya Mwaka (Alhamisi, Oktoba 12, 2017)  

Somo la 1

Mal. 3:13-18; 4:1-2

Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani? Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake. Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye. Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati yay eye amtumikiaye Mungu nay eye asiyemtumikia.

Kwa maana, angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru; na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake.


Wimbo wa Katikati

Zab. 1:1-4.6

Heri mtu yule asiyekwenda

Katika shauri la wasio haki;

Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;

Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.

Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, 

Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. 

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.


Naye atakuwa kama mti uliopandwa

Kandokando ya vijito vya maji,

Uzaao matunda yake kwa majira yake,

Wala jani lake halinyauki;

Na kila alitendalo litafanikiwa. 

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.


Sivyo walivyo wasio haki;

Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.

Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,

Bali njia ya wasio haki itapotea. 

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.


Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,

Pokeeni kwa upole neno la Mungu, lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.

Aleluya

Injili

Lk. 11:5-13

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nayi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au samaki, badala y asamaki atampa nyoka? Au akimwomba yai, atampa nge? Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Maoni


Ingia utoe maoni