Masomo ya Misa
Jumatano ya 27 ya Mwaka (Jumatano, Oktoba 11, 2017)
Yon. 4:1-11
Yona alikasirika sana. Akamwomba Bwana, akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya. Basi, sasa, Ee Bwana, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
Naye Bwana akasema, Je! Unatenda vema kukasirika? Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje. Na Bwana Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakauka.
Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Mungu akamwmbaia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili yam tango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa.
Bwana akamwmbia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuutesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja; na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tenda wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?
Zab. 86:3-6, 9-10
Wewe, Bwana, unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana.
(K) Wewe Bwana, u Mungu wa rehema na neema.
Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe.
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu.
(K) Wewe Bwana, u Mungu wa rehema na neema.
Mataifa yote uliwafanya watakuja;
Watakusujudia Wewe, Bwana.
Watalitukuza jina lako;
Kwa kuwa ndiwe uliye mkuu.
Wewe ndiwe mfanya miujiza,
Ndiwe Mungu peke yako.
(K) Wewe Bwana, u Mungu wa rehema na neema.
Ebr. 4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
Lk. 11:1 – 4
Yesu alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni: Baba, Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, Utupe siku kwa siku riziki yetu. Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni.
Maoni
Ingia utoe maoni