Masomo ya Misa
Dominika ya 12 ya Mwaka (Jumapili, Juni 25, 2017)
Yer. 20 : 10-13
Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo. nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji Katika mikono ya watu watendao maovu.
Zab. 69 : 7-9, 13,16, 32-34
Kwa ajili yako nimestahimili laumu,
Fedheha imenifunika uso wangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
Maana wivu wa nyumba yako umenila,
Na laumu yao wanaokulaumu zimenipata.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Nami maombi yangu nakuomba Wewe, Bwana,
Wakati ukupendezao; Ee Mungu,
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu,
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yetu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafunga wake.
Mbingu na nchi zimsifu
Bahari na vyote viendavyo ndani yake.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Rum. 5:12-15
Kama kwa mtu mmoja dhambi iliingia uli mwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi; maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria; walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, alive mfano wake yeye atakayekuja. Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.
Mdo. 16:14
Aleluya, aleluya,
Fungua mioyo yetu, ee Bwana,
Ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.
Mt. 10:26-33
Yesu aliwaambia mitume wake: Msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum, Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora nyinyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni