Masomo ya Misa
Jumatatu ya 11 ya MWaka (Jumatatu, Juni 19, 2017)
2 Kor. 6:1 – 10
Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi, msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa. Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, ktika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aisbu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali sikuzote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.
Zab. 98:1-4
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Efe. 1:17,18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Mt. 5:38 – 42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.
Maoni
Ingia utoe maoni