Masomo ya Misa
Jumamosi ya 9 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 09, 2017)
Tob. 11:5-15
Ana alikuwa amekaa kuyaelekeza macho yake njiani hali akimtazamia mwanawe. Akamwona mbwa akija mbio; akamwambia mumewe, Lo-o-o! Mwanao anakuja, na yule mtu aliyefuatana naye. Rafaeli akamwambia Tobia, Najua ya kuwa baba yako atafumbua macho yake. Basi umtie mara nyongo machoni; na imchomapo atajifikicha; na vyamba vyeupe vitaambuka; atakuona kwa macho. Lakini Ana alimkimbilia, akamwangukia mwanawe shingoni, akamwambia, Mwanangu! Nimekuona; tangu sasa ni radhi nife. Wakalia wote wawili. Tobiti naye akaondoka kwenda mlangoni, akajikwaa; lakini mwanawe akamkimbilia, akamshika baba yake; akamtia nyongo machoni, akasema, Jipe moyo, baba yangu. Yeye macho yake yalipoanza kuwasha aliyefikicha; navyo vyamba vyeupe vikaambuka katika pembe za macho yake, akamwona mwanawe, akamwangukia shingoni. Akalia, akasema, Ee Mungu umehimidiwa; na jina lako limehimidiwa milele; na watukuzwe malaika zako watakatifu wote. Kwa maana umenirudi, ukanihurumia; lo-o—o; namwona mwanangu Tobia.
Zab. 145:1,7-10
Aleluya.
Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Nitamsifu Bwana muda ninaoishi,
Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Au: Aleluya.
Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Au: Aleluya.
Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni;
Huwategemeza yatima na mjane.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Au: Aleluya.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, ee Sayuni,
Kizazi hata kizazi.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Au: Aleluya.
Zab. 111 :7, 8
Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.
Mk. 12:35-37
Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu, alijibu, akasema, Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe? Na mkutano mkubwa walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.
Maoni
Ingia utoe maoni