Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. FILIPO NERI (Ijumaa, Mei 26, 2017)
Mdo. 18: 9-18
Bwana alimwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu. Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema, Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi; bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo. Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu. Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu. Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.
Zab. 47:1-6
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Atawatiisha watu wa nchi chini yetu,
Na mataifa chini ya miguu yetu.
Atatuchagulia urithi wetu,
Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni.
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Yn- 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
Yn. 16:20-23
Siku ile Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika, lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.
Maoni
Ingia utoe maoni