Jumamosi. 21 Septemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 26, 2017

Ijumaa, Mei, 26, 2017,
Juma la 6 la Pasaka

Kumbukumbu ya Mt. Filipo Neri

Mdo 18: 9-18;
Zab 47: 2-7 (R. 8);
Yn 16: 20-23.


FURAHA NA TUMAINI LA UFUFUKO!

Kila tukio katika maisha yetu linaleta matokeo fulani katika maisha yetu. Wakati matokeo yakiwa mazuri tunakuwa na furaha. Na wakati tukiwa tunazamia mazuri yatokee hilo tunaita kuwa tumaini. Kama matokeo ni mabaya tunakuwa na huzuni na tunakuwa na hofu na mashaka. Hali hizi zinabadilika kadiri ya hisia zetu, na hayabakii kuwa yale yale. Injili inayaweka yote haya katika mfano wa kuzaliwa kwa mtoto. Kunakuwepo na maumivu, hofu lakini furaha huja baadae. Tunapaswa kuwenda zaidi ya haya tunayo yaona ulimwenguni ili tuweze kwenda kufuhia furaha ya ufalme wa Mungu. Kama Yesu alivyokufa juu ya vitu vyote ili afufuke katika utukufu wa Mungu, hivyo hivyo nasi tunapaswa tufe juu ya mambo yanayoleta furaha ya muda na kwa kufanya hivi lazima tuhizi uchungu wa kuacha baadhi ya mambo ili tuweze kufufuka ndani Yake. Maisha yanakuwa kwa kuyatoa, lakini yanaharibika kwa kujitenga na kujifariji binafsi.

Je, mateso yana maana kwamba upo mbali na Mungu? Au hauna neema ya Mungu? Ina maana kwamba Mungu amekuacha? Au ina maana kwamba unafanya kitu kibaya? Hakika sio hivyo, tunachopaswa kufanya nikuangalia maisha ya Yesu na tutatambua kwamba hili halipo hivyo. Alikuwa katika hali ya misuko suko na kupingwa na viongozi kila wakati lakini alijikita zaidi katika utume wa Baba yake. Alikuwa akisali kwa siku arobaini jangwani. Katika utume wake alikutana na vipingamizi vingi sana. Alitukanwa na kupingwa, kutokueleweka, kutemewa mate, na zaidi hata mpaka alivyokufa msalabani.

Mama yetu Bikira Maria alipatwa na “uchungu kama upanga” ukampenya moyo wake. Alikuwa na upendo kamili kwa mtoto wake. Aliwaona wengi waliokuwa wakimpenda mwanae na wale wasiompenda mwanae. Aliwaona wale waliokuwa wakimsulubisha na kumbebesha msalaba.

Lakini fikiria juu ya maisha yao. Wanafurahi sasa Mbinguni kama watakatifu, na Mama yetu kama Malkia wa mbinguni na watakatifu wote, na Yesu kama Mfalme wa Mbingu na Nchi. Wanaishi katika utukufu milele. Huzuni zao zimebadilika na kuwa furaha kamili. Kama unafikiri umetendewa vibaya au wamekuonea, furahi upo salama. Tambua kuwa unapo bakia mwaminifu na kutembea katika njia ya uaminifu ya Mungu aliokuwekea, mwisho ni kwamba utafurahia! Shikilia katika tumaini hilo na elekeza macho yako katika njia ya Mungu. Hakika utafanikiwa.

Sala: Bwana, ninakabidhi mizigo yangu yote na uchungu wote kwako. Ninaunganisha na msalaba wako nikitumaini kuwa utakuwa nami katika yote katika njia yangu ya maisha. Ninaomba niweke moyo wangu katika lengo langu nikiwa na furaha katika upendo wako kamili. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni