Masomo ya Misa
Alhamisi ya 2 ya Mwaka (Alhamisi, Januari 19, 2017)
Ebr. 7:25 – 8:6
Yesu aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengi, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele. Basi, aktika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu. Maana kila kuhani mkuu huwekwa ilia toe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa. Kama angekuwa juu ya nchi, asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria; watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima. Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.
Zab. 40: 6 – 9, 16
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
(K) Tazama nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Bwana.
Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
(K) Tazama nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Bwana.
Nimehubiri habari za haki, Katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu, Ee Bwana, unajua.
(K) Tazama nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Bwana.
2 Kor. 5:19
Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisha.
Aleluya.
Mk. 3:7-12
Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.
Maoni
Ingia utoe maoni