Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 2 ya Mwaka (Jumatano, Januari 18, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 7:1 – 3, 15 – 17

Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa Amani; hana baba, hana mama, mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, wewe u kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Wimbo wa Katikati

Zab. 110:1 – 4

Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkisedeki.


Bwana atainyosha toka Sayuni fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkisedeki.


Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako,
Kwa uzuri wa utkatifu,
Tokea tumbo la asubuhi,
Unao umande wa ujana wako.
(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkisedeki.


Bwana ameapa, wala hataghairi,
Ndiwe kuhani milele hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki.
(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkisedeki.

Shangilio

Yn. 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya, aleluya.

Injili

Mk. 3:1-6

Yesu aliingia katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki. Akawaambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati. Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.

Maoni


Ingia utoe maoni