Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 1 ya Mwaka (Alhamisi, Januari 12, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 3:7 – 14

Roho Mtakatifu asema: Leo, kama mtaisikia sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu, kama wakati wa kukasirisha, siku ya kujaribiwa katika jangwa, hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, wakaona matendo yangu miaka arobaini. Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; hawakuzijua njia zangu; kama nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho.

Wimbo wa Katikati

Zab. 95:6 – 11

Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu,
Kama vile huko Meriba, kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima wakayaona matendo yangu.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile,
Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo,
Hawakuzijua njia zangu.
Nikaapa kwa hasira yangu
Wasiingie rahani mwangu.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu.

Shangilio

Mt. 11:25

Aleluya, aleluya,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu nan chi, kwa kuw amambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Mk. 1:40-45

Siku ile mtu mwenye ukoma akaja kwa Yesu, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

Maoni


Ingia utoe maoni