Jumapili. 05 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Oktava ya Kuzaliwa Bwana (Alhamisi, Desemba 29, 2016)  

Somo la 1

1 Yoh 2:3-11

Wapenzi , Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake. Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda. Wapenzi, siwaandikii amri mpya, ila amri ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Na hiyo amri ya zamani ni neno lile mlilolisikia. Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung'aa. Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

Wimbo wa Katikati

Zab 96:1-3, 5-6

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Maana miungu yote ya watu si kitu,
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
Heshima na adhama ziko mbele zake,
Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.

Injili

Lk 2:22-35

Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.

Maoni


Ingia utoe maoni