Masomo ya Misa
SIKUKUU YA FAMILIA TAKATIFU YA YESU, MARIA NA YOSE (Ijumaa, Desemba 30, 2016)
Ybs. 3:2-6, 12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana, na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake huweka akiba iliyo azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; Kwa maana sadaka apewayo baba haitasahauliwa, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukuthibitisha.
Zab. 128:1-5
Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia zake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni,
Wakiizunguka meza yako.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake.
Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana,
Bwana akakubariki toka Sayuni.
Uone uheri wa Yerusalemu,
Siku zote za maisha yako.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana, aendaye katika njia zake.
Kol. 3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na Amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
Kol. 3:15,16
Aleluya, aleluya.
Na Amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu.
Aleluya.
Mt. 2:13-15, 19-23
Mamajusi walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya, akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.
Maoni
Ingia utoe maoni