Masomo ya Misa
Alhamisi ya 23 ya Mwaka (Alhamisi, Septemba 12, 2024)
1Kor 8:1-7, 11-13
Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga. Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lolote bado, kama impasavyo kujua. Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye. Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, nay a kuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa yeye huyo. Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika. Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake. Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhambiri iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo. Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.
Zab 139:1-3, 13-14, 23-24
Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze, Bwana, katika njia ya milele.
Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
(K) Uniongoze, Bwana, katika njia ya milele.
Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu,
Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu,
Ukaniongoze katika njia ya milele.
(K) Uniongoze, Bwana, katika njia ya milele.
Zab 147:12,15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
Lk 6:27-38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
Maoni
Ingia utoe maoni